Jumapili, 30 Juni 2013

Namna ya kutekeleza uzalishaji wa vifaranga bora


Chagua samaki wazazi wazuri kulingana na umbile lao kama rangi, ukubwa, afya na sura zao. Samaki hawa watengwe na wale wasio na sifa hizo na wasiruhusiwe kuzaliana nao. Mfugaji anaweza kununua wazazi hawa kutoka katika chanzo kinachofahamika kuwa kina samaki bora. 

Dhibiti ubora wa samaki hawa wazazi kwa kutoruhusu miingiliano na samaki wenye ubora hafifu. Chuja vema maji yanayoingia bwawa. Ikiwezekana, tumia samaki wenye ukubwa wa zaidi ya gramu 100. Hii itakuwezesha kutenganisha wazazi kutoka kwa vifaranga kila baada ya kuzaliwa (reproduction cycle).

Endelea kuwatumia wazazi hawa kila unapohitaji vifaranga kutegemeana na jinsi wanavyoendelea kuzaa vifaranga bora. Pamoja na ubora wa wazazi hawa, kuna umuhimu wa kuchagua na kuwaondoa vifaranga wasio kuwa na ubora unaohitajika au ambao ubora wao unatiliwa mashaka (culling).

Ni muhimu mfugaji afahamu uzuri wa kutumia vifaranga bora. Kausha bwawa kabisa angalau mara moja kila baada ya miezi sita hadi nane ili kuondokana na samaki wasio na ubora unao hitajika, kuua maadui wa samaki na kuondokana na hali ya kuwa na samaki wengi kwenye bwawa zaidi ya kiwango kinachotakiwa na pia hali ya samaki kuzaliana kinasaba “inbreeding”.  “Culling na grading” ni muhimu kuanza baada ya siku 30 hadi 45 baada ya samaki wakubwa kuwa wamewekwa kwenye bwawa na hufanyika kwa kutumia kawavu kadogo ambacho kina matundu madogo.
Endelea kufanya kazi hii kila baada ya wiki mbili hadi nne.

Urutubishaji wa bwawa na ulishaji wa samaki

Mfugaji anashauriwa kuweka mbaleo ya asili kama Mbuji  na samadi kwenye maji kabla ya kupandikiza samaki. Hii ni muhimu kwani samaki watakaopandikizwa, watahitaji chakula siku hiyo hiyo na chakula chao cha awali huwa ni vijimea na vijidudu vilivyomo ndani ya maji. Vyote hivi huwepo kwa wingi kwenye maji yenye rutuba.

Iwapo maji yatakuwa yamerutubishwa vema, chakula cha ziada huhitajika kwa kiasi kidogo sana, kama (2-3%) ya uzito wa samaki husika kwa siku. Ni vema samaki wakalishwa angalau mara mbili, kiasi kidogo asubuhi ya kati ya saa tatu na nne na jioni kati ya saa 10 na 11. Pia ni vema kama eneo la kulishia ikawa ni sehemu moja ili kuwazoesha samaki kuja eneo hilo muda wa kulisha na kuwawezesha kula sehemu kubwa ya chakula watakachopewa.     

KUZALIANA KWA WINGI NDANI YA BWAWA NA NJIA ZA KUDHIBITI


Kuwepo kwa samaki wengi kuliko idadi inayotakiwa ndani ya bwawa (overpopulation in ponds)
  1. Kwa kawaida, samaki jamii ya perege wako katika makundi mawili kutegemeana na wanavyo tunza mayai/watoto wao wakati wa kuzaliana. Perege jamii ya Oreochromis aureus, O. mossambicus na O. niloticus hutaga kwenye viota lakini hutunza mayai/vifaranga vyao midomoni kwa ajili ya kuyalinda dhidi ya maadui.
  2. Perege wa jamii ya T. rendalli na T. zilli hutaga na kutunza mayai/vifaranga vyao kwenye viota vinavyochimbwa na dume na jike kwa pamoja. Hulinda mayai/vifaranga vyao wakiwa kwenye viota na si kuwatunza kwenye midomo mdomoni panapotokea hatari.
  3. Urahisi wa jinsi wanavyo zaliana ni moja ya sababu inayofanya perege afae kwa ajili ya kufugwa kirahisi. Lakini, tabia hii pia husababisha matatizo. Uwezekano wa kukuza vifaranga wengi ni mkubwa na husababisha kuwepo samaki wengi kwenye bwawa kuliko uwezo wa bwawa.  Matokeo yake samaki hudumaa kutokana na uhaba wa chakula, hewa na hata sehemu za mapumziko. Katika hali hii, kuna uwezekano mkubwa kukuta samaki zaidi ya asilimia 75% wakiwa na ukubwa wa chini ya uzito wa gramu 100. Kwa maeneo ambayo samaki wadogo huliwa, hili linawezekana lisiwe tatizo, lakini kama lengo ni kuuza na kujipatia fedha, samaki wa ukubwa huu huuzika kwa taabu au kwa hasara. Katika kuzuia hali hiyo ya kudumaa samaki isitokee, yafuatayo huweza kufanyika:


Njia za kuweza kudhibiti uwingi wa perege kutokea kwenye bwawa
  1. Uvunaji wa mara kwa mara wa vifaranga kwa kutumia wavu. Njia hii hufaa kwenye bwawa dogo, ina shuruba na haihitaji uzoefu ili vifaranga wasife kutokana na majeraha watakaopata wakati wa kuwavua.
  2. Kutenganisha jinsia baada ya vifaranga kuwa na ukubwa wa kuweza kutenganishwa (monosex culture
  3. Kwa kawaida, madume hukua haraka kuliko majike. Hivyo, wengi hupendelea kufuga madume
  4. Kazi ya kutenganisha huweza kufanywa na mfugaji yeyote baada ya kuonyeshwa tofauti iliyopo kati ya jinsia moja na nyinge. Mkulima anashauriwa amuone mtaalam wa uvuvi aliye karibu naye kwa maelekezo.
  5. Katika mchakato wa kuwatenganisha, makosa huweza kufanyika na kusababisha baadhi ya jinsia tofauti kutotenganishwa, mkulima asikate tamaa kwani idadi itakayokuwa imetenganishwa bado itatoa tija nzuri.
  6. Kupandikiza vifaranga machotara (stocking hybrid "all-male" fingerlings: Madume hukua haraka kuliko majike
  7. Utahitaji samaki wazazi waliohakikiwa ubora wake (requires pure strains of broodstock.
  8. Utahitaji sehemu maalum ya kuzalishia na mtaalam aliyefuzu.
  9. Ili kukidhi mahitaji ya vifaranga wa perege kwa wafugaji, kuna umuhimu wa wafugaji binafsi kuanzisha “hatcheries” kwa ajili ya kuzalisha vifaranga bora na kuwauzia wengine wenye kuhitaji. Japo kuwa kwa sasa baadhi ya wafugaji huzalisha vifaranga na kuwauzia au kuwagawia wenzi wao, wafugaji hazalisha vifaranga hao kama sehemu ya uzalishaji wa samaki wa kawaida kwenye bwawa. Kwa kadiri shughuli hii inavyokuwa, wafugaji wengi hupendelea kupata vifaranga bora. Na kwa jinsi hii, “hatchery” itakayokuwa ikizalisha vifaranga bora itapata soko zuri la vifaranga wake.

UZALISHAJI WA VIFARANGA



Uchaguzi wa mbegu bora (wazazi)  
Samaki aina ya perege huzaliana wakati wote wa mwaka. Wana tabia ya kuzaa vifaranga wengi. Samaki
wazazi huweza kufugwa kwenye mabwawa au matanki wakiwa wanasubiri kuzaliana. Idadi ya mayai
yatakayotagwa na perege jike hutegemea ukubwa wa kimaumbile wa samaki jike. Kwa kawaida majike
wadogo hutaga mayai machache wakati wale wakubwa hutaga mayai mengi. Hii hutokana na uwezo wa
tumbo kuweza kubeba idadi ya mayai.

Inawezekana kutofautisha perege dume na jike kwa urahisi wanapokuwa na uzito wa gramu 15. Perege
jike ana tundu moja katikati ya mapezi matatu yaliyo karibu na mwisho wa mkia eneo la tumboni. Kwa
upande wa dume eneo hilo hilo kuna mrija uliojitokeza kwa nje.

Uzalianaji wa perege
Kama ilivyokwisha elezwa hapo juu, perege ni moja ya aina ya samaki ambao huweza kuzaliana kwenye
maji yaliyozingirwa (captivity) kama vile bwawa la kuchimbwa na hata tenki.
          
Ili mfugaji atape mbegu bora, ni vema akaanda mazingira mazuri yatakayopelekea kupatikana kwa
mbegu (vifaranga) bora. Hatua zifuatazo ni muhimu:

  1. Chagua samaki wazazi na kuwaweka kwenye bwawa au tenki uliloliandaa kwa kuzalishia vifaranga. Uwiano unaopendekezwa ni wa samaki majike 2 kwa dume 1. Huyo dume mmoja ana uwezo wa kurutubisha mayai ya majike hayo2. Ukiweka madume wengi, watakuwa wakigombana wao kwa wao badala ya kuzaliana. Chagua samaki wenye ukubwa na umbo linalofaa na linalopendeza.
  2. Mara tu baada ya vifaranga kuanguliwa huweza kuogelea wakiwa wamejichukulia kiini cha yai (yolk sack) ambacho hutumika kama chakula kwa muda wa siku 2 –3. Baada ya hapo, vifaranga uanza kujilisha vimelea (planktons) vitakavyokuwa vikipatikana ndani ya maji. Baada ya muda, vifaranga hao watakuwa na uwezo wa kuendelea kula vimelea hivyo, vijidudu na hata chakula cha ziada kama pumba za mahindi, za mpunga kama watapewa kama chakula cha ziada. Waachwe wakue kwa muda wa wiki tatu au zaidi kabla ya kuwahamisha kwenda kwenye bwawa la kukuzia. Kwa kuwa vifaranga hawa watakuwa na umri mmoja (ni wa rika moja), ukubwa sawa na ni wachanga, watakuwa na uwezo mkubwa wa kukua kwa ubora zaidi.

UHIFADHI WA MBEGU KWA AJILI YA MZUNGOKO MWINGINE WA UPANDAJI SAMAKI BWAWANI NA MATATIZO KATIKA UFUGAJI SAMAKI..


Unapovuna samaki, hakikisha kuwa vifaranga au samaki wazazi utakaokuwa umewachagua wanawekwa katika kijibwawa kingine (kinachojulikana kama nursery pond) kabla ya kuwarudisha bwawa la kukuzia (production pond). Ni muhimu kufanyia bwawa matengenezo na kulijaza maji kabla ya kuweka samaki tena. Hili ni muhimu kwa mfugaji kwani kinamhakikishia mfugaji kujua kuwa anapanda mbegu changa na ambao  hawajadumaa. Pia humhakikishia kujua kuwa samaki waliopandwa wanalingana na ujazo wa bwawa, yaani vifaranga viwili kwa kila mita moja ya mraba na pia hurahisisha maji ya bwawa kurutubika kirahisi.

MATATIZO YA UFUGAJI SAMAKI
Ingawa ufugaji wa samaki si kazi ngumu sana, kuna matatizo mbali mbali ambayo mfugaji anaweza 
kukumbana nayo. Lakini, matatizo mengi yanaweza kuepukika kama mfugaji ataweza kufuata kikamilifu 
maelekezo ya ujengaji na utunzaji wa bwawa.
  1. Tatizo mojawapo ni la kuvuja kwa kuta za bwawa. Tatizo hili hutokea iwapo ujengaji wa bwawa haukufuata maagizo na taratibu za ujengaji wa bwawa. Iwapo utakumbana na tatizo hili, muone afisa uvuvi aliye karibu nawe upate ushauri.
  2. Tatizo la maadui wa samaki kama vile ndege, kenge, fisi maji, nyoka hutokea. Kwa kiasi kikubwa tatizo hili huambatana na ujengaji bwawa mbali na nyumbani na bwawa kuwa na nyasi nyingi (halifyekewi). Suluhisho ni kufweka nyasi kila mara, kujenga uzio kwa kutumia matete na hata nyaya za seny’enge, kuwinda ndege na kuharibu mazalia/maskani yao, bwawa kuwa karibu na maskani ya watu.
  3. Kudumaa kwa samaki kutokana na kuwa wengi bwawani kupita idadi inayotakiwa. Tatizo hili hutokana na kutokukaushwa bwawa kwa kipindi kirefu. Utatuzi huweza kuwa; kukausha bwawa kila baada ya miezi 6 hadi 9
  4. Ugumu wa kukausha maji bwawani. Husababishwa na bwawa kujenjwa kwenye eneo la tambarare kiasi kuwa hakuna uwezekano wa kutumia bomba au kukata kuta za bwawa kuondoa maji. Utatuzi; chimba bwawa kwenye eneo lenye mteremko wa wastani
  5. Bwawa lisilo kaushika huwa mazalia ya Mbu wakati linapokuwa halina samaki ndani yake na kusaidia kuenea kwa malaria. Konokono wenye mabuu ya kichocho huzaliana kwenye mabwawa yenye kina kifupi au yenye majani mengi. Ni vema kuwa na bwawa yenye kina cha kutosha, lisilo na nyasi au majani ndani yake na linaloweza kukaushika kirahisi ili kuondokana na matatizo haya.

Matunzo, uvunaji wa samaki na zana ziazotumika kuvulia samaki


MATUNZO YA SAMAKI BWAWANI.

Ili bwawa liweze kutoa samaki wazuri muda wote yafaa bwawa la samaki lihudumiwe kwa kufuata 
maelekezo yafuatayo;
  1. Angalia samaki wanavyoogelea na kula wakati unapowalisha. Kama hawana matatizo, watajitokeza juu kwa wingi na kula vizuri kwa furaha.
  2. Ondoa magugu na mimea katika bwawa.
  3. Fyeka majani kando kando ya bwawa.
  4. Angalia kila siku kiasi cha maji kama yananywea au hayanywei, yanatosha au hayatoshi.
  5. Angalia rangi ya maji ili ujue kama unahitaji kuongeza mbolea.
  6. Chunguza kama kuna ndege na wanyama waharibifu na ukiwabaini, wadhibiti mapema.


UVUNAJI WA SAMAKI. 

Wakati wa kufaa kuvuna samaki bwawani hutegemea ukuaji na aina ya samaki. Ukuaji wa samaki pia hutegemea wanavyokula, wingi wao bwawani na joto la maji. Samaki wanakuwa haraka kwenye maji ya joto kuliko kwenye maji ya baridi. Pia mfugaji mwenye bidii ya kulisha na kutunza bwawa, samaki wake watakua haraka. Samaki wanaofugwa katika bwawa lenye hali nzuri watakuwa tayari kuvunwa baada ya miezi 6 hadi 9.
Ni ukweli usiopingika kuwa; kwa kadiri juhudi na maarifa yanavyoongezwa katika bwawa, ndivyo kiasi cha samaki kitakachovunwa kitakavyoongezeka.

ZANA ZITUMIKAZO KATIKA UVUNAJI SAMAKI
  
Kwa kawaida, kuna makusudi mawili ya kuvuna samaki waliofugwa bwawani:
  1. Kwa ajili ya kitoweo au kiasi kidogo kwa ajili ya kuuza.
  2. Uvunaji wa samaki wote ili kuhitimisha msimu mmoja wa ufugaji samaki.
Kwa samaki wachache wa mboga au kuuza, unaweza kutumia kipande cha nyavu, mitego ya asili (migono), ndoano na hata kipande cha nguo. Kwa uvunaji wa samaki wote ili kuhitimisha msimu wa ufugaji, njia nzuri ni kuondoa maji yote kutoka katika bwawa   na kukamata samaki wote mara moja. Unaweza kuondoa maji kwa namna mbili:
  • Kukata ukuta ulio upande wa kina kirefu, weka chujio ili kuzuia samaki kutoka halafu ruhusu maji kutoka.
  • Kutumia bomba la kuondolea maji kwa kufunikwa na kipande cha nyavu au kitu cho chote kisichoruhusu samaki kutoka bwawani isipokuwa maji.
Njia hii ni muhimu kwani isipofanyika kwa kipindi kirefu, samaki watakuwa wengi mno bwawani na kusababisha wengi kudumaa na kuwa na umbo dogo.
Samaki wanaofugwa bwawani huweza kuliwa wabichi baada ya kupikwa, kuchomwa, kukaangwa au kuuzwa kwa wanaohitaji.
Mfugaji pia anaweza kuuza samaki wachanga (vifaranga) kwa watu wenye kuhitaji mbegu za kupanda.
Baadhi ya samaki wakubwa wanaweza kukaushwa kwa moto, moshi, jua au kutiwa chumvi ili wasiharibike au kuoza upesi. Hii ni katika kuwahifadhi.

URUTUBISHAJI WA BWAWA LA SAMAKI KWA MBOLEA NA (MAJIVU) PAMOJA NA USAFIRISHAJI WA VIFARANGA WA SAMAKI.


  1. Kutegemea aina ya udongo, majivu ya moto huweza kutawanywa bwawani kabla ya kuingiza maji ili kupunguza Tindikali ya udongo na kuua baadhi ya wadudu walio maadui wa samaki waliopo katika eneo la bwawa.
  2. Mbolea huweza kutawanywa bwawani kabla ya kuweka maji ili kusaidia kujenga mazingira ya maji kutuama (yaani Kushikamanisha udongo).
  3. Vinginevyo, mbolea huwekwa eneo maalum (Uzio) mara baada ya maji kuingizwa bwawani ili kulirutubisha na Kuliwezesha liwe na vijimea na vijidudu vidogo vidogo vitakavyokuwa chakula cha awali cha samaki.
  4. Dalili za kuwepo kwa vijimelea hivyo bwawani ni kugeuka rangi ya maji na kuwa ya kijani.
  5. Aina ya mbolea hutegemea upatikanaji wake. Samadi ya ng’ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe, kuku, bata na hata Majani mabichi yaozayo kirahisi na yasiyo sumu kwa wanyama na binadamu huweza kutumika.
  6. Kiasi cha kuweka mbolea hutegemea sana ukubwa wa bwawa, aina ya samadi na idadi ya samaki waliomo.
  7. Kipimo kizuri cha kiasi kinachotosha ni kuingiza mkono ndani ya maji hadi kufikia kwenye kiwiko, na usipoona Kiganja chako, basi simamisha uwekaji wa mbolea kwani vijimelea na vijidudu waliomo wanatosha kulisha samaki Waliomo kwenye bwawa kwa muda wa siku kadhaa.
  8. Ukizidisha mbolea ni hatari kwa samaki, kwani wanaweza kufa kwa kukosa hewa ya oksijeni, hasa nyakati za usiku.



Usafirishaji, upandaji na ulishaji wa vifaranga wa samaki

USAFIRISHAJI WA VIFARANGA WA SAMAKI
Upatapo vifaranga, visafirishe wakati wa asubuhi kwa kutumia ndoo ya plastiki, chungu, maplastiki makubwa.

Weka kiasi cha vifaranga 200 katika ndoo moja. Ni vema mkulima kuwa na tabia ya kupunguza maji 
kwenye ndoo yenye samaki na kuweka mengine afikapo eneo lenye maji.

Ufikapo bwawani, inamisha ndoo ili maji ya kwenye ndoo yaingiliane na yale ya bwawani. 
Hii ni kuruhusu joto la maji na mazingira ya maji yaingiliane na kuwa sawa.

Waruhusu samaki watoke bwawani wenyewe bila ya kuwamwaga. Itachukuwa muda kabla ya vifaranga wote kuingia bwawani. Kwa kufanya hivyo, samaki hawatapata mshituko ambao wanaweza kupata kama 
watamwagwa. Mshituko wa   ghafla huweza kusababisha vifo.


UPANDAJI WA VIFARANGA VYA SAMAKI.
Ubora wa samaki utakao wafuga utategemea sana ubora wa vifaranga utakaokuwa umepanda bwawani.

Chanzo chako cha vifaranga ni bora kiwe na vifaranga wenye umri mdogo na ambao hawajadumaa.

Kwa samaki aina ya Perege, panda vifaranga viwili (2) hadi watatu (3) kwa kila mita moja ya mraba.

Kwa sasa,  samaki aina ya Perege ndio wanaoshauriwa kufugwa na wafugaji wa maji baridi hapa nchini.

Kambale huweza kufugwa na mkulima mzoefu kwani huduma yake huitaji mtaji mkubwa katika 
kuwalisha na Utaalam katika kuzalisha vifaranga vyake.


ULISHAJI WA SAMAKI.

  1. Samaki, Kama walivyo wanyama wengine, wanahitaji kula.
  2. Chakula cha samaki huweza kugawanywa katika makundi mawili:-
  3. Cha asili kipatikanacho ndani ya bwawa kama vile vijimea, vijidudu na samaki wadogo.
  4. Cha ziada ambacho huongezwa bwawani na mkulima.
  5. Ili chakula cha asili kipatikane bwawani, ni vema bwawa liwe limerutubishwa vizuri, kwani vijimea vinavyotarajiwa humea palipo na rutuba.
  6. Chakula za ziada huwekwa bwawani na mkulima mwenyewe. Aina ya chakula cha ziada hutegemea upatikanaji wake, gharama na aina na ukubwa wa samaki. Baadhi ya chakula cha ziada ni kama: pumba za mahindi, za mpunga, mashudu ya pamba na karanga, machicha ya pombe, ugali na masazo ya jikoni, baadhi ya majani pori, majani yatokayo bustanini.
  7. Inashauriwa mfugaji alishe kila siku, kwa muda ule ule, saa ile ile na sehemu ile ile. Tabia hii hujenga mazoea ya samaki kula zaidi na kupunguza wingi wa chakula kinachopotea.
  8. Usilishe chakula kingi zaidi ya mahitaji ya samaki kwa siku hiyo. Mfano, usiweke debe zima la pumba kwa mara   moja na kuacha kulisha kwa wiki nzima! Sehemu ya chakula kitakachosalia, kitaoza na baadhi ya siku samaki hawatakuwa na chakula, watashinda na kulala njaa!




Jumamosi, 29 Juni 2013

UCHAGUZI WA ENEO LINALOFAA KWA AJILI YA KUCHIMBA BWAWA LA SAMAKI.


Ni jambo muhimu sana kuchagua eneo zuri ili kurahisisha na kufanikisha kwa urahisi kazi ya  kufuga samaki. Si kila eneo la ardhi hufaa kwa kazi ya kufuga samaki. Eneo zuri kwa ufugaji samaki ni eneo lenye maji ya kutosha na ya kuaminika, udongo unaotuamisha maji (mfinyanzi), ikiwezekana pawepo mtelemko wa kiasi.

  1.  Maji ya kutosha ni yale yanayoweza kujaza bwawa lako ndani ya siku chache. Pia maji hayo yawe ni ya kuaminika ili wakati unapoyahitaji, yapatikane. Chanzo chaweza kuwa mto au chemichemi. (Maji ya mvua hayaaminiki, wakati yale ya bomba ni ya ghali sana kutokana na kuyalipia kwa mamlaka husika).
  2. Udongo unaofaa ni ule unaotuamisha maji, kama vile wa mfinyanzi au mchanganyiko wa mfinyanzi na tifutifu. Mchanga mtupu haufai kwani huruhusu maji kunywea kirahisi.
  3. Mteremko ni vema usiwe mkali sana, ila uwezeshe maji kutiririka kuingia na kutoka bwawani. Eneo la tambarare kabisa si zuri sana, kwani utafanya uchimbaji wa bwawa kuwa kama kisima na haitakuwa rahisi kuondoa maji toka bwawani itakapo hitajika  ambalo si zuri kwa ufugaji bora wa samaki.
  4. Ni vizuri eneo liwe karibu na nyumbani ili kudhibiti wezi na maadui wa samaki, pia huwezesha kutoa huduma kwa urahisi.


CHAGUO LA UMBO NA UKUBWA WA BWAWA
  1. Umbo na ukubwa wa bwawa hutegemea sura na mwinuko wa eneo husika na eneo alilonalo mfugaji.
  2. Kwa kawaida umbo lolote hufaa kwa uchimbaji wa bwawa, lakini, ili kurahisisha uvunaji, umbo mraba au mstatili upendekezwa zaidi.
  3. Vile vile, ukubwa wa bwawa hutegemea ukubwa wa eneo husika, uwingi wa maji na uwezo wa mkulima.
  4.  Bali, ili kupata pato la kuridhisha na kurahisisha utoaji huduma kama vile kulisha, inapendekezwa kuwa ukubwa wa bwawa ni vema liwe na upana wa kati ya mita 10 na mita 20 na urefu wa kati ya mita 20 na mita 30. Umbo la mraba au mstatili huvutuia zaidi.

Hatua za muhimu katika uchimbaji wa bwawa
  • Fyeka mahali pa kujenga bwawa.
  • Pima bwawa na weka mambo.
  • Ondoa udongo wa juu (mbolea, mchanga, mizizi n.k.) na weka pembeni.
  • Chimba msingi wa kuta; upana futi 1 na kina futi 1½.
  • Jaza huo msingi kwa udongo wa mfinyanzi na kuushindilia. Hii itasaidia kupunguza kunywea kwa maji.
  • Anza kuchimba bwawa na kujenga kuta kwa kutumia udongo tu (bila mchanga, mawe, miti, mizizi n.k.) ili kupunguza kunywea kwa maji kutoka bwawani baada ya kulijaza.
  • Shindilia kikamilifu udongo unaowekwa kwenye kuta.
  • Jaribu kusawazisha juu ya kuta na chonga kuta ziwe na mtelemko wa kiasi, zisiwe wima kwani zitamomonyoka kirahisi.
  • Chonga sakafu ya bwawa kwa kuiwekea mteremko wa kiasi kutoka upande wenye kina kifupi kwenda upande wenye kina kirefu..
  • Weka bomba la kuingizia maji na bomba la kuondolea maji bwawani.
  • Rudishia udongo wa juu uliouondoa hapo awali kwenye kuta za bwawa.
  • Panda majani yanayotambaa  kama mbudu ukutani kuzuia mmomonyoko.
  • Jenga wigo wa kuweka mbolea ya samadi au Mbuji ndani yake
  • Jenga uzio, seng’enge au panda miti yenye miba kuzunguka bwawa kuzuia maadui wa samaki kuingia bwawani.
  • Tawanya mbolea na majivu chini ya bwawa ili kuua wadudu wanaoweza kuwamo ndani ya bwawa kabla ya samaki kupandwa bwawani.
  • Baada ya hatua hizo kukamilika, sasa jaza maji bwawani.

UFUGAJI WA PEREGE

Ufugaji wa samaki
Ufugaji samaki ni kazi ya kupanda, kukuza na kutunza samaki katika mabwawa au uzio (uliotengenezwa kwa vyuma, nyavu 
au miti) au eneo lolote ambalo udhibiti wake yako chini ya mamlaka ya mfugaji mwenyewe. Mabwawa yaweza kuwa ni ya 
kuchimbwa na watu (japokuwa ya asili pia huweza kutumika) wakati uzo inaweza ikawa imewekwa katika eneo lolote 
lililo na maji kama ziwa na hata bahari.
Ufugaji samaki kwa kiasi fulani si sawa na ukuaji samaki katika mito, maziwa na bahari. Tofauti iko katika huduma inayotolewa kwa samaki wafugwao na idadi ya samaki wanaopaswa kuwamo ndani ya eneo husika. Samaki waliofugwa huhitaji kulishwa na kuhudumiwa.
Ufugaji wa samaki si kitu kipya kabisa hapa Tanzania. Baadhi ya Watanzania wamekuwa wakifuga samaki katika mabwawa 
hata kabla ya nchi yetu kupata uhuru. Lakini baadhi ya wafugaji wamekuwa wakitoa matunzo hafifu kiasi cha kufanya 
mavuno kutokuwa mazuri. Kwa miaka ya karibuni, serikali imetilia mkazo utoaji elimu (ugani) wa ufugaji samaki ili 
kuboresha mafanikio yake. Kuchapishwa kwa kitabu hiki kitasaidia kuongeza uelewa wa wakulima wafugaji wa 
samaki katika shughuli nzima ya ufugaji samaki nchini.

Faida za ufugaji samaki
Ufugaji samaki una faida nyingi sana, baadhi ni haya:
1.  Chakula bora chenye uto-mwili (protini) muhimu inayohitajika kujenga mwili.
2.  Kujipatia kipato baada ya kuuza samaki waliofugwa.
3.  Kuboresha kazi nyingine za kilimo kama bustani ya mboga, ufugaji wa ng’ombe, bata, kuku, nguruwe, bustani ya miti, n.k.
4.  Huwezesha kutumia rasilimali ambayo isingekuwa ikitumika kama kusingekuwa na ufugaji samaki kama vile eneo 
     la ardhi lenye maji maji, pumba za mahindi na mpunga, na mabaki ya mboga mboga kutoka bustanini kwa kulishia samaki.
5.  Eneo la bwawa huwa ni sehemu nzuri ya mapumziko.
  
Hatua muhimu katika shughuli za ufugaji samaki
1.     Uchaguzi wa mahala panapofaa kwa ajili ya kuchimba bwawa la samaki.
2.     Tathmini ya umbo na ukubwa wa bwawa
3.     Uchimbaji wa bwawa.
4.     Uingizaji na utoaji wa maji katika bwawa.
5.     Uwekaji wa mbolea na (majivu).
6.     Upandaji wa vifaranga vya samaki.
7.     Ulishaji wa samaki na matunzo mengine bwawani.
8.     Uvunaji wa samaki na aina ya nyavu/zana zifaazo kutumika.
9.     Uhifadhi wa mbegu kwa ajili ya mzungoko mwingine wa upandaji samaki bwawani.

Vigezo muhimu katika kuboresha uzalishaji 
Joto au ubaridi wa maji katika sehemu husika huweza kuongeza au kupunguza hamu ya ulaji wa samaki na hivyo ukuaji wake. 
  • Chakula cha samaki (cha asili na cha ziada), aina ya chakula na kiasi kinachopatikana.
  • Uwingi wa samaki waliomo bwawani kulinganisha na ukubwa wa bwawa.
  • Ubora wa vifaranga (quality) waliopandwa. Vifaranga wenye ubora mruzi huwa na uwezo wa kukua haraka.
  • Muda uliotumika kuzalisha samaki. Japokuwa samaki hukua haraka, wanahitaji muda wa kutosha kufikia ukubwa unaofaa kwa mahitaji ya mkulima au wa soko. 
  • Uwepo wa magugu na mimea isiyohitajika bwawani.
  • Uwepo wa maadui wa samaki (predators).
  • Kuwa na tabia ya kuvua bwawa kila baada ya miezi 6 hadi 9 kwa kulikausha ili kuboresha mazingira yake.
  • Huduma inayotolewa bwawani husaidia  kupatikana samaki wakubwa na wenye afya.







Aquatic weeds as potential feed for Tilapia

Women Farmers In Tanzania Get Ahead With Fishponds And Irrigation Canals

Global Fish Farming News: Tanzania

Tanzania woes citizens to invest infish farming