Jumamosi, 29 Juni 2013

UCHAGUZI WA ENEO LINALOFAA KWA AJILI YA KUCHIMBA BWAWA LA SAMAKI.


Ni jambo muhimu sana kuchagua eneo zuri ili kurahisisha na kufanikisha kwa urahisi kazi ya  kufuga samaki. Si kila eneo la ardhi hufaa kwa kazi ya kufuga samaki. Eneo zuri kwa ufugaji samaki ni eneo lenye maji ya kutosha na ya kuaminika, udongo unaotuamisha maji (mfinyanzi), ikiwezekana pawepo mtelemko wa kiasi.

  1.  Maji ya kutosha ni yale yanayoweza kujaza bwawa lako ndani ya siku chache. Pia maji hayo yawe ni ya kuaminika ili wakati unapoyahitaji, yapatikane. Chanzo chaweza kuwa mto au chemichemi. (Maji ya mvua hayaaminiki, wakati yale ya bomba ni ya ghali sana kutokana na kuyalipia kwa mamlaka husika).
  2. Udongo unaofaa ni ule unaotuamisha maji, kama vile wa mfinyanzi au mchanganyiko wa mfinyanzi na tifutifu. Mchanga mtupu haufai kwani huruhusu maji kunywea kirahisi.
  3. Mteremko ni vema usiwe mkali sana, ila uwezeshe maji kutiririka kuingia na kutoka bwawani. Eneo la tambarare kabisa si zuri sana, kwani utafanya uchimbaji wa bwawa kuwa kama kisima na haitakuwa rahisi kuondoa maji toka bwawani itakapo hitajika  ambalo si zuri kwa ufugaji bora wa samaki.
  4. Ni vizuri eneo liwe karibu na nyumbani ili kudhibiti wezi na maadui wa samaki, pia huwezesha kutoa huduma kwa urahisi.


CHAGUO LA UMBO NA UKUBWA WA BWAWA
  1. Umbo na ukubwa wa bwawa hutegemea sura na mwinuko wa eneo husika na eneo alilonalo mfugaji.
  2. Kwa kawaida umbo lolote hufaa kwa uchimbaji wa bwawa, lakini, ili kurahisisha uvunaji, umbo mraba au mstatili upendekezwa zaidi.
  3. Vile vile, ukubwa wa bwawa hutegemea ukubwa wa eneo husika, uwingi wa maji na uwezo wa mkulima.
  4.  Bali, ili kupata pato la kuridhisha na kurahisisha utoaji huduma kama vile kulisha, inapendekezwa kuwa ukubwa wa bwawa ni vema liwe na upana wa kati ya mita 10 na mita 20 na urefu wa kati ya mita 20 na mita 30. Umbo la mraba au mstatili huvutuia zaidi.

Hatua za muhimu katika uchimbaji wa bwawa
  • Fyeka mahali pa kujenga bwawa.
  • Pima bwawa na weka mambo.
  • Ondoa udongo wa juu (mbolea, mchanga, mizizi n.k.) na weka pembeni.
  • Chimba msingi wa kuta; upana futi 1 na kina futi 1½.
  • Jaza huo msingi kwa udongo wa mfinyanzi na kuushindilia. Hii itasaidia kupunguza kunywea kwa maji.
  • Anza kuchimba bwawa na kujenga kuta kwa kutumia udongo tu (bila mchanga, mawe, miti, mizizi n.k.) ili kupunguza kunywea kwa maji kutoka bwawani baada ya kulijaza.
  • Shindilia kikamilifu udongo unaowekwa kwenye kuta.
  • Jaribu kusawazisha juu ya kuta na chonga kuta ziwe na mtelemko wa kiasi, zisiwe wima kwani zitamomonyoka kirahisi.
  • Chonga sakafu ya bwawa kwa kuiwekea mteremko wa kiasi kutoka upande wenye kina kifupi kwenda upande wenye kina kirefu..
  • Weka bomba la kuingizia maji na bomba la kuondolea maji bwawani.
  • Rudishia udongo wa juu uliouondoa hapo awali kwenye kuta za bwawa.
  • Panda majani yanayotambaa  kama mbudu ukutani kuzuia mmomonyoko.
  • Jenga wigo wa kuweka mbolea ya samadi au Mbuji ndani yake
  • Jenga uzio, seng’enge au panda miti yenye miba kuzunguka bwawa kuzuia maadui wa samaki kuingia bwawani.
  • Tawanya mbolea na majivu chini ya bwawa ili kuua wadudu wanaoweza kuwamo ndani ya bwawa kabla ya samaki kupandwa bwawani.
  • Baada ya hatua hizo kukamilika, sasa jaza maji bwawani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni