Jumapili, 30 Juni 2013

Matunzo, uvunaji wa samaki na zana ziazotumika kuvulia samaki


MATUNZO YA SAMAKI BWAWANI.

Ili bwawa liweze kutoa samaki wazuri muda wote yafaa bwawa la samaki lihudumiwe kwa kufuata 
maelekezo yafuatayo;
  1. Angalia samaki wanavyoogelea na kula wakati unapowalisha. Kama hawana matatizo, watajitokeza juu kwa wingi na kula vizuri kwa furaha.
  2. Ondoa magugu na mimea katika bwawa.
  3. Fyeka majani kando kando ya bwawa.
  4. Angalia kila siku kiasi cha maji kama yananywea au hayanywei, yanatosha au hayatoshi.
  5. Angalia rangi ya maji ili ujue kama unahitaji kuongeza mbolea.
  6. Chunguza kama kuna ndege na wanyama waharibifu na ukiwabaini, wadhibiti mapema.


UVUNAJI WA SAMAKI. 

Wakati wa kufaa kuvuna samaki bwawani hutegemea ukuaji na aina ya samaki. Ukuaji wa samaki pia hutegemea wanavyokula, wingi wao bwawani na joto la maji. Samaki wanakuwa haraka kwenye maji ya joto kuliko kwenye maji ya baridi. Pia mfugaji mwenye bidii ya kulisha na kutunza bwawa, samaki wake watakua haraka. Samaki wanaofugwa katika bwawa lenye hali nzuri watakuwa tayari kuvunwa baada ya miezi 6 hadi 9.
Ni ukweli usiopingika kuwa; kwa kadiri juhudi na maarifa yanavyoongezwa katika bwawa, ndivyo kiasi cha samaki kitakachovunwa kitakavyoongezeka.

ZANA ZITUMIKAZO KATIKA UVUNAJI SAMAKI
  
Kwa kawaida, kuna makusudi mawili ya kuvuna samaki waliofugwa bwawani:
  1. Kwa ajili ya kitoweo au kiasi kidogo kwa ajili ya kuuza.
  2. Uvunaji wa samaki wote ili kuhitimisha msimu mmoja wa ufugaji samaki.
Kwa samaki wachache wa mboga au kuuza, unaweza kutumia kipande cha nyavu, mitego ya asili (migono), ndoano na hata kipande cha nguo. Kwa uvunaji wa samaki wote ili kuhitimisha msimu wa ufugaji, njia nzuri ni kuondoa maji yote kutoka katika bwawa   na kukamata samaki wote mara moja. Unaweza kuondoa maji kwa namna mbili:
  • Kukata ukuta ulio upande wa kina kirefu, weka chujio ili kuzuia samaki kutoka halafu ruhusu maji kutoka.
  • Kutumia bomba la kuondolea maji kwa kufunikwa na kipande cha nyavu au kitu cho chote kisichoruhusu samaki kutoka bwawani isipokuwa maji.
Njia hii ni muhimu kwani isipofanyika kwa kipindi kirefu, samaki watakuwa wengi mno bwawani na kusababisha wengi kudumaa na kuwa na umbo dogo.
Samaki wanaofugwa bwawani huweza kuliwa wabichi baada ya kupikwa, kuchomwa, kukaangwa au kuuzwa kwa wanaohitaji.
Mfugaji pia anaweza kuuza samaki wachanga (vifaranga) kwa watu wenye kuhitaji mbegu za kupanda.
Baadhi ya samaki wakubwa wanaweza kukaushwa kwa moto, moshi, jua au kutiwa chumvi ili wasiharibike au kuoza upesi. Hii ni katika kuwahifadhi.

Maoni 1 :

  1. Nataka mafunzo ya aquaponic agriculture

    JibuFuta