Jumapili, 30 Juni 2013

Namna ya kutekeleza uzalishaji wa vifaranga bora


Chagua samaki wazazi wazuri kulingana na umbile lao kama rangi, ukubwa, afya na sura zao. Samaki hawa watengwe na wale wasio na sifa hizo na wasiruhusiwe kuzaliana nao. Mfugaji anaweza kununua wazazi hawa kutoka katika chanzo kinachofahamika kuwa kina samaki bora. 

Dhibiti ubora wa samaki hawa wazazi kwa kutoruhusu miingiliano na samaki wenye ubora hafifu. Chuja vema maji yanayoingia bwawa. Ikiwezekana, tumia samaki wenye ukubwa wa zaidi ya gramu 100. Hii itakuwezesha kutenganisha wazazi kutoka kwa vifaranga kila baada ya kuzaliwa (reproduction cycle).

Endelea kuwatumia wazazi hawa kila unapohitaji vifaranga kutegemeana na jinsi wanavyoendelea kuzaa vifaranga bora. Pamoja na ubora wa wazazi hawa, kuna umuhimu wa kuchagua na kuwaondoa vifaranga wasio kuwa na ubora unaohitajika au ambao ubora wao unatiliwa mashaka (culling).

Ni muhimu mfugaji afahamu uzuri wa kutumia vifaranga bora. Kausha bwawa kabisa angalau mara moja kila baada ya miezi sita hadi nane ili kuondokana na samaki wasio na ubora unao hitajika, kuua maadui wa samaki na kuondokana na hali ya kuwa na samaki wengi kwenye bwawa zaidi ya kiwango kinachotakiwa na pia hali ya samaki kuzaliana kinasaba “inbreeding”.  “Culling na grading” ni muhimu kuanza baada ya siku 30 hadi 45 baada ya samaki wakubwa kuwa wamewekwa kwenye bwawa na hufanyika kwa kutumia kawavu kadogo ambacho kina matundu madogo.
Endelea kufanya kazi hii kila baada ya wiki mbili hadi nne.

Urutubishaji wa bwawa na ulishaji wa samaki

Mfugaji anashauriwa kuweka mbaleo ya asili kama Mbuji  na samadi kwenye maji kabla ya kupandikiza samaki. Hii ni muhimu kwani samaki watakaopandikizwa, watahitaji chakula siku hiyo hiyo na chakula chao cha awali huwa ni vijimea na vijidudu vilivyomo ndani ya maji. Vyote hivi huwepo kwa wingi kwenye maji yenye rutuba.

Iwapo maji yatakuwa yamerutubishwa vema, chakula cha ziada huhitajika kwa kiasi kidogo sana, kama (2-3%) ya uzito wa samaki husika kwa siku. Ni vema samaki wakalishwa angalau mara mbili, kiasi kidogo asubuhi ya kati ya saa tatu na nne na jioni kati ya saa 10 na 11. Pia ni vema kama eneo la kulishia ikawa ni sehemu moja ili kuwazoesha samaki kuja eneo hilo muda wa kulisha na kuwawezesha kula sehemu kubwa ya chakula watakachopewa.     

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni